WANANCHI WA KIPUMBWI NA USHONGO WAPATA ELIMU YA TAHADHARI ZA EL NINO*
Wananchi wa vijiji vya Kipumbwi na Ushongo, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, wamepata elimu kuhusu tahadhari wanazopaswa kuchukua ili kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua za vuli na hali ya El Nino.
Elimu hiyo imetolewa leo Septemba 26, 2026, na Kaimu Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Tanga, Brackley Millenium, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usalama wa wadau wa usafiri majini.
“Tunawahimiza wavuvi, mabaharia, wamiliki wa vyombo na abiria kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa kabla ya kuanza safari, pia, wahakikishe vyombo vinakaguliwa na vina vifaa muhimu vya kuokoa maisha,” amesema Millenium.
Ameongeza kuwa tahadhari hizo zikizingatiwa zitasaidia kuzuia ajali, kulinda maisha na mali pamoja na kuhakikisha shughuli za uvuvi na usafiri majini zinafanyika kwa usalama.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kipumbwi, Sabiri Omari, amewataka wananchi kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na wataalamu wa TASAC.
“Elimu hii ni muhimu kwa usalama wetu. Ninawasihi wananchi wote kuzingatia na kufuata maelekezo tuliyopewa ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza,” amesema Omari.
Naye, Juma Khamis Salum, ambaye ni miongoni mwa wananchi waliopokea elimu hiyo, ameishukuru TASAC na kuahidi kuitumia katika shughuli zake za uvuvi.
“Nitakwenda kutekeleza yote niliyofundishwa ili nijilinde na kuwalinda wengine dhidi ya athari za El Nino wakati wa shughuli zangu uvuvi,” amesema Salum.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Ushongo wameishukuru TASAC kwa kuwapatia elimu hiyo, wakisema itawasaidia kufanya shughuli za uvuvi na usafiri majini kwa tahadhari zaidi, hususan wakati wa mvua za vuli na hali ya El Nino.