Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WAFANYAKAZI WA TASAC WAANZA MAZOEZI YA PAMOJA

Imewekwa: 17 August, 2026
WAFANYAKAZI WA TASAC WAANZA MAZOEZI YA PAMOJA

Wafanyakazi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kupitia TASAC Sports Club, tarehe 14 Agosti 2026 wameanza rasmi mazoezi ya pamoja yenye lengo la kuimarisha afya, utimamu wa mwili, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi.

Mazoezi hayo yaliongozwa na Meneja Rasilimali Watu wa TASAC, Bi. Pili Mazoewa, kuanzia katika Sanamu la Askari Samora Posta, jijini Dar es Salaam, na kuendelea hadi Fukwe za Coco (Coco Beach), ambapo washiriki walifanya mazoezi na kutembea kwa pamoja.

Akizungumza wakati wa mazoezi hayo, Bi. Mazoewa alisema kuwa mpango huo, ulioanzishwa na TASAC SPORTS CLUB, ni sehemu ya jitihada za taasisi kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa na afya bora na mazingira mazuri ya kufanya kazi.

“Afya ya mfanyakazi ni muhimu sana katika kuongeza ufanisi na tija kazini. Tunataka kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, si kwa ajili ya afya ya mwili pekee, bali pia kuimarisha umoja, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi,” alisema Bi. Mazoewa.

Aidha, Bi. Mazoewa aliwahimiza wafanyakazi wote kushiriki kikamilifu katika programu hiyo, akisisitiza kuwa kuwa na mwili wenye afya ni msingi muhimu wa kujenga nguvu kazi yenye ari, uwezo na ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

Kwa upande wao wafanyakazi walionesha hamasa na ushirikiano mkubwa wakati wa zoezi hilo, hali inayoashiria utayari wa kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi na kuimarisha mshikamano ndani ya TASAC.

Mazoezi hayo yaliyoanzishwa na TASAC Sports Club yatafanyika kila Ijumaa kuanzia saa 11:15 jioni, yakianzia Sanamu la Askari Samora Posta hadi Fukwe za Coco (Coco Beach).

Mrejesho, Malalamiko au Wazo