TAHADHARI YA EL NIÑO: WAVUVI NA WAFANYABIASHARA BANDARI YA KIBIRIZI WAASWA KUCHUKUA TAHADHARI
Wavuvi, wafanyabiashara na wadau wengine wanaofanya shughuli zao katika eneo la Bandari ya Kibirizi mkoani Kigoma wameaswa kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa katika msimu wa Vuli 2026.
Wito huo umetolewa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kupitia elimu ya usalama kwa wadau wa usafiri na shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika maeneo ya bandari na kwenye Ziwa Tanganyika.
Akizungumza wakati wa mkutano wa uhamasishaji uliofanyika katika Bandari ya Uvuvi Kibirizi, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kigoma, Nahodha Adam Mamilo amewataka wavuvi na waendeshaji wa vyombo vya usafiri majini kuhakikisha vyombo vyao vinakuwa katika hali salama na vina vifaa muhimu vya uokoaji kabla ya kuanza safari.
Nahodha Mamilo amewahimizwa wadau hao kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kabla ya kwenda ziwani, na kuepuka kufanya safari au shughuli za uvuvi wakati hali ya hewa ni hatarishi.
Kwa upande wa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya bandari, Nahodha Mamilo amewata kuzingatia usalama wa mali na bidhaa zao, kuweka bidhaa katika maeneo salama na kuchukua hatua za mapema pale kunapokuwa na viashiria vya mvua kubwa, upepo mkali au kuongezeka kwa kina cha maji.
Kwa mujibu wa TMA msimu wa Vuli wa Oktoba hadi Desemba 2026 unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño, huku maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma yakitarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Aidha, Serikali imeelekeza wananchi na taasisi kuchukua hatua za mapema za kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwa ni pamoja na kutambua maeneo hatarishi, kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuhakikisha mifumo ya dharura na vifaa vya uokoaji inakuwa tayari.