Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WADAU WA USAFIRI WILAYA YA UKEREWE WAASWA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA EL NIÑO

Imewekwa: 07 September, 2026
WADAU WA USAFIRI WILAYA YA UKEREWE WAASWA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA EL NIÑO

Wadau wa usafiri kwa njia ya maji katika Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, wameaswa kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali ya hewa ya El Niño inayotarajiwa kuathiri msimu wa mvua za Vuli 2026, kwa kuzingatia taarifa rasmi iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Wito huo umetolewa na Afisa Mfawidhi (OIC) wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Wilaya ya Ukerewe, Naho. Michael Rogers, wakati wa semina ya utoaji elimu kwa wadau wa usafiri majini kuhusu kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali hiyo ya hewa. Semina hiyo imefanyika tarehe 6 Septemba, 2026, katika mialo mbalimbali iliyopo Kata ya Bwiro, Wilaya ya Ukerewe.

Naho. Rogers amesema kuwa, katika kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazoambatana na El Niño, ni wajibu wa kila mmiliki na mtumiaji wa chombo cha usafiri majini kuhakikisha chombo kinakuwa na vifaa vyote muhimu vya usalama kabla ya kuanza safari.

Amesisitiza umuhimu wa kuwa na vifaa vya kuokoa maisha, hususan jaketi okozi, pamoja na kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika ipasavyo wakati wote wa safari.

“Ni muhimu kwa kila anayefanya kazi katika chombo kuhakikisha chombo kimesajiliwa na TASAC na kina vyeti halali ambavyo havijaisha muda wake. Aidha, chombo kinapaswa kuwa na jaketi okozi za kutosha na kuhakikisha watumiaji wanazivaa wakati wote wanapokuwa safarini,” alisema Naho. Rogers.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ukerewe, SGT Salasala Buluba, amewasihi wananchi na wadau wa usafiri majini kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa kabla na wakati wa safari, pamoja na kuzingatia maelekezo ya usalama yanayotolewa na mamlaka husika.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kuepuka kusafiri wakati hali ya hewa si salama, ili kulinda maisha ya wasafiri na watumiaji wengine wa vyombo vya usafiri majini.

“Naishukuru TASAC kwa kuendelea kutoa elimu mara kwa mara. Hii inaonyesha jinsi TASAC inavyothamini na kujali maisha ya Watanzania. Jeshi la Polisi lipo bega kwa bega na TASAC katika kusimamia sheria za usafiri majini kwa lengo la kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika. Usalama wako na wa abiria ni jukumu letu sote, hivyo kila mmoja wetu hana budi kuchukua tahadhari,” alisema SGT Buluba.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo