WADAU MBALIMBALI WATEMBELEA BANDA LA TASAC KATIKA MAONESHO YA WIKI YA MADINI GEITA
Wananchi na wadau mbalimbali wametembelea Banda la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) katika Maonesho ya Wiki ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, Mkoani Geita.
Katika banda hilo, wananchi na wadau wamepata fursa ya kufahamishwa kuhusu majukumu ya TASAC katika kusimamia na kudhibiti shughuli za wakala wa meli, pamoja na utekelezaji wa majukumu yake kwa kuzingatia weledi, ufanisi na uwajibikaji.
Maelezo hayo yametolewa na Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Geita (OIC), Nahodha Godfrey Chegere, ambaye ameeleza kuwa TASAC ina jukumu la kusimamia usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira katika sekta ya usafiri majini. Aidha, ameeleza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika katika kusimamia na kuendeleza sekta ya usafiri majini.
Wadau hao pia wamepata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu mchango wa TASAC katika kuhakikisha usafiri salama na endelevu majini, pamoja na jitihada za Shirika za kutoa elimu kwa umma kuhusu uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia shughuli za usafiri majini.
Aidha, wananchi wamepata elimu kuhusu jukumu la TASAC katika ugomboaji na uondoshaji wa shehena zinazoingizwa au kutolewa nchini kwa bidhaa maalum zenye maslahi mapana kwa nchi na taifa kwa ujumla. Bidhaa hizo ni pamoja na silaha na vilipuzi, makinikia, kemikali zinazotumika katika kampuni za uchimbaji madini, nyara za Serikali na wanyama hai kama ilivyoainishwa katika sheria husika za uhifadhi wa wanyamapori.
Wadau pia wamekumbushwa kuchukua tahadhari kutokana na matarajio ya mvua za Vuli zinazotarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi wa Septemba hadi Desemba 2026, ambazo zinatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na El Niño.
Maonesho ya Wiki ya Madini yameanza Septemba 23, 2026, na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 3, 2026.