Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TAWI LA COTWU (T) – TASAC LAFANYA MKUTANO WA MWAKA NA UCHAGUZI MKUU

Imewekwa: 27 September, 2026
TAWI LA COTWU (T) – TASAC LAFANYA MKUTANO WA MWAKA NA UCHAGUZI MKUU

Tawi la Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU–T) la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), tarehe 25 Septemba 2026 lilifanya Mkutano Mkuu wa Tawi kwa lengo la kujadili masuala ya ustawi wa wafanyakazi pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wa Tawi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akizungumza katika Mkutano huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Hamid Mbegu, amewaahidi wajumbe ushirikiano, umoja na mshikamano, pamoja na kufanya kazi kwa ukaribu na Menejimenti ya Shirika ili kuimarisha ushirikiano, kuongeza tija na ufanisi wa utendaji kazi na kuhakikisha TASAC inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa COTWU (T), Bi. Juliana Mpanduji, amewahimiza wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi na mawasiliano kujiunga na COTWU–Tanzania ili kuwa na sauti moja katika kutetea maslahi yao mahali pa kazi na kunufaika na Mkataba wa Hali Bora.

Kabla ya uchaguzi, Katibu wa Tawi la COTWU (T) – TASAC, Nahodha George Mnali, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Tawi kwa kipindi cha miaka mitano na kujibu hoja mbalimbali za wanachama.

Katika uchaguzi huo, Bw. Mohamed Kapera amechaguliwa kuwa Mwenyekiti na Nahodha George Mnali kuwa Katibu wa COTWU (T) – TASAC. Wajumbe wa Kamati Tendaji waliochaguliwa ni Hashimu Awadh, Salma Mohamed, Nahodha David Chiragi, Nahodha Mzee Mvihanga, Juma Mwacha na Chester Kapinga.

Aidha, Bi. Martha Ngasha amechaguliwa kuwa Mjumbe Maalum Mwanamke; Mhandisi Kelvin Kami, Mwenyekiti wa Vijana; Aggrey Koni, Katibu wa Vijana; huku Richard Nyasenga na Wilfred Chawene wakiwa Wajumbe wa Kamati ya Vijana.

Kwa upande wa Wanawake, CPA Edda Mwakatobe amechaguliwa kuwa Mwenyekiti na Florence Marick kuwa Katibu, huku Selina Mokiti na Victoria Myonga wakiwa Wajumbe wa Kamati ya Wanawake.

Akizungumza baada ya uchaguzi, Mwenyekiti mpya, Bw. Kapera aliahidi kufanya kazi kwa ukaribu na menejimenti ili kuendeleza umoja, mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Shirika na kulinda maslahi ya wafanyakazi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo