TASAC YAWAJENGEA UWEZO WADAU WA USAFIRI MAJINI PANGANI KUKABILIANA NA EL NINO
Wadau wa usafiri majini katika Kata ya Pangani Mashariki mkoani Tanga wamejengewa uelewa kuhusu hatua za kufuata ili kuendelea na shughuli zao kwa usalama wakati wa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi yanayoweza kujitokeza katika kipindi cha El Nino.
Elimu hiyo imetolewa Septemba 25, 2026, na Afisa Mwandamizi wa Udhibiti na Usimamizi kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Tanga, Patrick Nungwe, kwa wananchi, wavuvi, wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri majini.
“Safari salama inaanza na uamuzi sahihi kabla ya kuingia majini, kila mdau anapaswa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kusitisha safari iwapo kuna dalili za upepo mkali, mvua kubwa au mawimbi hatarishi,” amesema Nungwe.
Amesisitiza kuwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo wanapaswa kukagua hali ya vyombo vyao na kuhakikisha vifaa vya kuokoa maisha vinapatikana na vinatosheleza idadi ya watu waliomo ndani ya chombo.
Mtendaji wa Kata ya Pangani Mashariki, Rajabu Shame, amewahimiza wananchi kutopuuzia matumizi ya jaketi okozi na kuhakikisha kila msafiri anavaa kwa usahihi kabla ya safari kuanza.
“Jaketi okozi si mzigo wa kubebwa ndani ya chombo, bali ni kinga muhimu inayopaswa kuvaliwa, elimu tuliyoipata itumike kulinda maisha yetu na ya watu tunaowasafirisha,” amesema Shame.
Naye, Afisa Uvuvi wa Kata ya Pangani Mashariki, Rashidi Rashid, amewataka wavuvi kutanguliza usalama badala ya kuhatarisha maisha kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.
“Uvuvi ni muhimu kwa maisha na uchumi wetu, lakini hakuna samaki mwenye thamani kuliko uhai, hali ya hewa inapokuwa mbaya, ni busara kusubiri hadi mazingira yatakapokuwa salama,” amesema Rashid.