Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC yatoa tuzo kwa wanafunzi bora NIT

Imewekwa: 18 January, 2024
TASAC yatoa tuzo kwa wanafunzi bora NIT

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekabidhi tuzo kwa wanafunzi bora wa shahada ya kwanza ya  Usafirishaji Mizigo na Usimamizi wa Bandari,  Astashahada ya Uhandisi wa Ijenzi na Matengenezo Meli na Astashahada ya Upakuaji na Upakiaji wa Shehena  katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT). 

Utoaji wa tuzo hizo umefanyika katika mahafali ya 22 ya chuo cha bandari
sambamba na kongamano la 10 lililoandaliwa na NIT tarehe 8 Disemba, 2023 ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma wa Mabasi ya Mwendokasi (UDART) Bw.Gilliard Ngewe.

Akifungua kongamano hilo Bw. Gilliard Ngewe alisema "wanafunzi  mnahitimu maisha ya chuo na mnakuja kwenye jamii kutumia maarifa mliyoyapata kutoka chuoni hapa. Taifa letu liko mabegani mwenu. Mtaendelea kujifunza maisha na kuboresha maarifa mliyopata hadi kuwa wabobezi wa taaluma mlizojifunza".

Naye makamu Mkuu wa Chuo Dkt.Zainabu Mshana amesema kuwa Chuo hicho kinaandaa wataalam kimkakati ili kukidhi uhitaji wa jamii katika kuinua maendeleo ya nchi. 

"Tutaendelea kuwapa motisha wanachuo waendelee kufanya vizuri kwa kushirikiana na wadau" amesema Dkt. Mshana

TASAC iliwakilishwa na Nicholous Kinyariri, Afisa  Uhusiano kwa Umma kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo na kukabidhi tuzo kwa wanafunzi hao.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo