Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YATOA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO MAHALA PA KAZI

Imewekwa: 29 September, 2026
TASAC YATOA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO MAHALA PA KAZI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa mafunzo ya kupambana na majanga ya moto mahala pa kazi kwa watumishi wake, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kinadharia na vitendo kuhusu namna ya kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika Ukumbi wa City Garden, Dar es Salaam, Afisa Tawala Mkuu, Bw. Dollar Kusenge, amesema mafunzo hayo yataongeza uelewa wa watumishi kuhusu aina mbalimbali za moto, namna ya kutumia vifaa vya kuzimia moto na taratibu sahihi za kuchukua hatua wakati wa dharura, mahala pa kazi na hata nyumbani.

“Kupitia mafunzo haya, mtajifunza kuhusu aina mbalimbali za moto, mbinu za kuuzima pamoja na taratibu za kuchukua wakati wa dharura, hatua ambazo zitasaidia kupunguza hatari ya maafa yanayoweza kutokea kutokana na majanga ya moto,” amesema Bw. Kusenge.

Ameongeza kuwa TASAC inatarajia kuwa, baada ya mafunzo hayo, watumishi watakuwa na uelewa na utayari zaidi wa kukabiliana na majanga ya moto, ikiwa ni pamoja na kutambua vihatarishi vya moto, kutumia kwa usahihi vifaa vya kuzimia moto na kuchukua hatua stahiki wakati wa dharura.

Kwa mujibu wa Bw. Kusenge, mafunzo hayo pia ni sehemu ya juhudi za TASAC katika kuimarisha usalama na afya mahala pa kazi, pamoja na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na majanga ya moto.

Mafunzo hayo yanatolewa kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Tanzania na yameanza leo, tarehe 28 Septemba 2026, na yanatarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba 2026.

Jumla ya watumishi takribani 280 wanatarajiwa kushiriki na kunufaika na mafunzo hayo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo