TASAC YATOA ELIMU YA TAHADHARI YA EL NINO KWA WADAU WA USAFIRI MAJINI MKOANI TANGA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mkoa wa Tanga, limetoa elimu kuhusu tahadhari za usalama kwa wadau wa usafiri majini katika Ufukwe wa Petukiza, Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga, kufuatia matarajio ya kuanza kwa mvua za vuli na uwezekano wa kutokea kwa hali ya El Niño.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Tanga, Nahodha David Chiragi, amewataka wamiliki wa vyombo vya majini, mabaharia, wavuvi na abiria kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa kabla na wakati wa safari ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Tunawakumbusha wadau wote kuwa usalama huanza kabla ya safari. Ni muhimu kufuatilia taarifa za hali ya hewa, kukagua vyombo vyao na kuepuka kuingia majini pale hali ya hewa inapoonekana kuwa si salama,” amesema Nahodha Chiragi.
Aidha, amewasisitiza wamiliki wa vyombo vya majini kuhakikisha vyombo vyao viko katika hali nzuri, vina vifaa vya mawasiliano vinavyofanya kazi na vina vifaa vya kutosha vya kuokoa maisha, hususan jaketi okozi. Pia, amewataka kuzingatia uwezo na idadi ya abiria pamoja na kiwango cha mzigo kinachoruhusiwa, na kuepuka upakiaji wa kupita kiasi.
“Usalama wa maisha ya watu ni jukumu la kila mmoja. Hakuna safari yenye umuhimu kuliko uhai. Kila abiria anapaswa kuvaa jaketi okozi. Jaketi okozi si pambo la kuwekwa ndani ya chombo, bali ni kifaa muhimu cha kuokoa maisha wakati wa dharura. Kila chombo kinapaswa pia kuzingatia idadi ya abiria iliyoidhinishwa,” amesisitiza.
Kwa upande wao, wananchi na wadau wa usafiri majini katika Ufukwe wa Petukiza wameishukuru TASAC kwa kuwapatia elimu hiyo kwa wakati, wakieleza kuwa itawasaidia kuchukua tahadhari na kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuanza safari au shughuli za uvuvi.
“Tumefurahi kupata elimu hii kwa wakati. Tutaendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuhakikisha tunazingatia matumizi ya jaketi okozi ili kulinda maisha yetu,” amesema mmoja wa wananchi walioshiriki katika elimu hiyo.