TASAC YASHIRIKI MKUTANO WA PILI WA KIMATAIFA WA LOJISTIKI NA UCHUKUZI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeshiriki Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Lojistiki na Uchukuzi unaofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City Jijini Dar es salaam leo tarehe 17 Oktoba, 2024.
Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), ambaye katika hotuba yake ya ufunguzi amesema Serikali inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 600 kwa ajili ya kugharamia miradi mitatu itakayoboresha huduma ya usafirishaji kwa njia ya maji mkoani Kigoma na maeneo yanayozunguka.
Mhe. Prof. Mbarawa amesema miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha meli, ujenzi wa meli ya mizigo pamoja na meli ya kisasa ya abiria inayotarajiwa kufanya safari zake katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria.
“Bandari ya Kigoma ni muhimu kwa sababu kwenye Ziwa Tanganyika tunapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kule kuna madini, kutokana na hilo kama Serikali tumeona tuweke nguvu za kutosha katika kuhakikisha tunatumia Bandari ya Kigoma ipasavyo kwa kujenga vyombo vya kisasa,”amesema Mhe. Prof. Mbarawa.
Aidha ameongeza kuwa, kiwanda cha meli kinategemewa kujenga meli za kisasa huku ujenzi wa meli ya kisasa ya abiria inayotarajiwa kubeba kati ya abiria 600 mpaka 900 na meli ya mizigo inayotarajiwa kubeba tani 3,000 za mizigo ambapo itakuwa pia na njia za magari kwa mfumo wa mlango kwa mlango.
“Miradi hii yote ambayo itaanza hivi karibuni na itagharimu kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 600 ambapo itaboresha suala la usafirishaji katika Bandari ya Kigoma, kubwa zaidi ni kujenga meli ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia watu, kukamilika kwa ujenzi huu wa meli kutaleta ajira, kufungua sekta ya usafirishaji, na kukuza uchumi,”amesema Mhe. Prof. Mbarawa.
Kwa upande Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amewaasa washiriki wa mkutano huo kuhakikisha wanatumia fursa hii kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya uchukuzi ili kupata muafaka wa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
TASAC ni mmoja wa wadhamini wa mkutano huo wa siku tatu uliofunguliwa rasmi leo, na kufikia kilele chake tarehe 19 Oktoba, 2024.