TASAC YASHIRIKI MKUTANO WA NNE WA KIMATAIFA WA USAFIRISHAJI, LOJISTIKI NA USIMAMIZI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeshiriki katika Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Usafirishaji, Lojistiki na Usimamizi (ICTLM 2026), uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Mkutano huo umewakutanisha wadau kutoka sekta za usafirishaji, lojistiki, biashara na uchukuzi kwa lengo la kujadili fursa, changamoto na maendeleo katika sekta hizo, pamoja na kubadilishana uzoefu na maarifa yatakayochochea ufanisi na ukuaji wa uchumi.
Sambamba na mkutano huo, yamefanyika maonesho yaliyoshirikisha taasisi na mashirika mbalimbali. Kupitia maonesho hayo, washiriki wamepata fursa ya kutangaza huduma zao na kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu na shughuli zinazotekelezwa na taasisi zao.
TASAC imeshiriki katika maonesho hayo kupitia banda lake, ambalo limekuwa kivutio kwa wageni na wadau mbalimbali waliotembelea kupata elimu na ufafanuzi kuhusu majukumu ya Shirika katika kusimamia na kudhibiti sekta ya usafiri majini nchini.
Wageni waliotembelea banda hilo wameelimishwa kuhusu usalama na ulinzi wa usafiri majini, utunzaji wa mazingira ya majini, usajili na ukaguzi wa vyombo, mafunzo na uthibitishaji wa mabaharia, pamoja na udhibiti wa huduma za usafirishaji majini na biashara ya meli.
Aidha, wadau wamepata ufafanuzi kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya usafiri majini na umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vinavyolenga kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa usalama, ufanisi na ushindani.
Ushiriki wa TASAC katika ICTLM 2026 umeendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Shirika na wadau wa sekta za lojistiki na usafirishaji. Pia, umetoa fursa kwa TASAC kuendelea kujenga uelewa wa umma kuhusu majukumu yake na mchango wa sekta ya usafiri majini katika maendeleo ya biashara na uchumi wa Taifa.
Mkutano na maonesho hayo ya siku mbili yalianza tarehe 20 Agosti, 2026 na kuhitimishwa leo tarehe 21 Agosti, 2026.