Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YASHIRIKI KONGAMANO LA TANO LA KITAIFA LA MEL WEEK 2026

Imewekwa: 25 September, 2026
TASAC YASHIRIKI KONGAMANO LA TANO LA KITAIFA LA MEL WEEK 2026

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linashiriki katika Kongamano la Tano la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL Week 2026), linalofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 26 Septemba 2026 katika Hoteli ya Ngurdoto Mountain Lodge, jijini Arusha.

TASAC ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika kongamano hilo na pia ni mmoja wa wadhamini wa tukio hilo, hatua inayoonesha dhamira ya Shirika katika kuunga mkono juhudi za kujenga utamaduni wa ufuatiliaji, tathmini, kujifunza na matumizi ya takwimu katika kuboresha utendaji wa taasisi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, TASAC inapata fursa ya kuwafikia wadau mbalimbali na kuwafahamisha kuhusu majukumu, huduma na shughuli zinazotekelezwa na Shirika katika sekta ya usafiri wa majini nchini.

Aidha, kongamano hilo linatoa fursa kwa TASAC kushirikishana uzoefu na wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) katika kuhakikisha taasisi zinafanya maamuzi yanayozingatia ushahidi, kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

TASAC inawakaribisha washiriki wa kongamano hilo, wadau wa sekta ya usafiri wa majini, taasisi za Serikali, mashirika, wataalamu na wananchi kutembelea banda la TASAC katika eneo la maonesho ili kupata taarifa zaidi kuhusu Shirika, huduma zake na namna linavyoshirikiana na wadau katika kuendeleza sekta ya usafiri wa majini nchini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo