TASAC YASHINDA NAFASI YA KWANZA KWA UNUNUZI WA UMMA KWENYE KUNDI LA WIZARA, IDARA NA WAKALA WA SERIKALI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeshinda tuzo ya mshindi wa kwanza katika Utendaji Bora Katika Ununuzi kwa Kuzingatiaji Sheria na Thamani ya Fedha kwenye kundi la Wizara, Idara na Wakala wa Serikali (MDA’s)
Tuzo hiyo imetolewa leo tarehe 29 Julai, 2026 jijini Arusha katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Ndg. Toba Nguvila kwa niaba ya Waziri wa Fedha.
Akitoa hotuba kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Nguvila ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya PPRA kwa kazi nzuri wanayoifanya. “Naipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA na Menejimenti kwa kazi inayofanyika katika kusimamia na kudhibiti shughuli za ununuzi wa umma”. Amesema Nguvila.
Pia amesema kuwa ununuzi wa umma na ugani sio tu utaratibu wa kupata bidhaa, huduma na kazi za ujenzi pekee, bali ni nyenzo ya kisera na kimkakati ya serikali katika kuchochea uzalishaji na ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira, kuimarisha kampuni za ndani, kukuza ubunifu na kuhakikisha maendeleo yananufaisha watanzania wengi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Ndg. Nelson Mlali ameishukuru PPRA kwa usimamizi mzuri wa ununuzi wa umma ambao umeleta tija kwa Taifa. Ameongeza kwa kusema kuwa, TASAC itaendelea kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na serikali ili kupata thamani halisi ya fedha na uadilifu katika ununuzi wa umma.
Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma la mwaka 2026 limeanza leo tarehe 29 Julai, 2026 na litakamilika tarehe 31 Julai, 2026. Kaulimbiu ya kongamano ni Kutumia Fursa za Ununuzi wa Umma Kidijitali Kufikia Uchumi Endelevu, Jumuishi na Shindani Kuelekea Dira ya Taifa 2050.