Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAKUTANISHA WADAU TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUJADILI MAPENDEKEZO YA KUJIUNGA NA ITIFAKI ZA USALAMA WA MELI ZA MWAKA 1988

Imewekwa: 26 November, 2026
TASAC YAKUTANISHA WADAU TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUJADILI MAPENDEKEZO YA KUJIUNGA NA ITIFAKI ZA USALAMA WA MELI ZA MWAKA 1988

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekutana na wadau wa sekta ya usafiri majini kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kukusanya maoni kuhusu mapendekezo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujiunga na Itifaki za mwaka 1988 za Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Maisha Baharini (SOLAS) na Mkataba wa Kimataifa wa Mistari ya Ukomo wa Upakiaji wa Meli (Load Lines). Vikao hivyo vimefanyika Dar es Salaam na Zanzibar kwa nyakati tofauti.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bi. Elizabeth Masawe, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kisheria, kitaasisi na kiutendaji katika usimamizi wa usalama wa meli, sambamba na uwekezaji wa Serikali katika kuboresha miundombinu na huduma za bandari. Amesema sekta ya usafiri majini ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na biashara ya kimataifa, hivyo ni muhimu kuzingatia viwango vya kimataifa vya usalama.

Aidha, amesema kujiunga na Itifaki hizo kutaiwezesha Tanzania kuoanisha taratibu za ukaguzi, tathmini na utoaji wa vyeti vya meli kupitia Mfumo Ulioratibiwa wa Ukaguzi, Tathmini na Utoaji wa Vyeti vya Meli (Harmonised System of Survey and Certification – HSSC), ambao utapunguza urudufu wa ukaguzi, muda na gharama za kiutendaji, huku ukiimarisha wajibu wa Tanzania kama nchi ya bendera na nchi ya bandari.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Ramadhan Omar Mohammed, amesema TASAC na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) zina wajibu wa kuhakikisha sekta ya usafiri majini inazingatia viwango vya kimataifa, ili kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa baharini duniani, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TASAC, Bi. Judith Kakongwe, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau katika kutoa maoni ili kuhakikisha mchakato huo unazingatia mahitaji ya sekta na mazingira halisi ya utekelezaji nchini.

Vikao hivyo ni sehemu ya mchakato wa Serikali wa kukusanya maoni kabla ya kufanya uamuzi kuhusu kujiunga na Itifaki hizo, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa meli, ufanisi wa huduma za usafiri majini na ushindani wa bandari za Tanzania katika biashara ya kimataifa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo