Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAKUTANA NA WADAU KUPOKEA MAONI YA MAOMBI YA MAPITIO YA TOZO YALIYOWASILISHWA NA TPA

Imewekwa: 11 December, 2025
TASAC YAKUTANA NA WADAU KUPOKEA MAONI YA MAOMBI YA MAPITIO YA TOZO YALIYOWASILISHWA NA TPA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 11 Desemba, 2025, limekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri wa majini kwa ajili ya kupokea maoni kuhusu maombi ya mapitio ya tozo za bandari za bahari yaliyowasilishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). 

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amesema kuwa kikao hiki ni sehemu muhimu ya mchakato wa mapitio ya tozo kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha Sheria ya TASAC, Sura ya 415, kinachoitaka TASAC kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufanya uamuzi wowote wa kupitisha tozo au viwango vya huduma. 

Bw. Salum amebainisha kuwa maombi yaliyowasilishwa na TPA yametimiza matakwa ya Kanuni za Tozo za TASAC za mwaka 2020, hivyo kufanya kikao hiko kuwa hatua rasmi ya majadiliano ili kuzingatia maslahi mapana ya wadau ikiwemo ufanisi wa bandari, ushindani wa kikanda, na gharama kwa watumiaji wa huduma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa, amesema kuwa mapitio hayo yanatokana na baadhi ya tozo hazijafanyiwa marekebisho kwa zaidi ya miaka kumi, huku huduma nyingine zikiendelea kutolewa bila kutozwa licha ya kuwa na gharama kubwa za uendeshaji. 

Bw. Mbossa amesisitiza kuwa marekebisho haya yamelenga kuhakikisha bandari za Tanzania zinabaki shindani, zenye ufanisi na zenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo ya biashara ya kimataifa.

Katika majadiliano hayo, wadau wameainisha masuala muhimu kama athari za mapendekezo ya tozo kwa shughuli za biashara na uchukuzi, uwezo wa bandari kuhudumia mizigo kwa haraka, na umuhimu wa kuendelea kujenga mazingira bora na thabiti ya uwekezaji. 

TASAC inaendelea kukusanya na kuchambua maoni ya wadau kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina kabla ya kutoa mapendekezo ya mwisho kuhusu tozo husika. Maoni ya wadau yataendelea kupokelewa hadi tarehe 31 Desemba, 2025.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo