TASAC YAKUSANYA MAONI YA WADAU KUHUSU MAOMBI YA NAULI ZA MELI YA MV. LIEMBA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe Oktoba 20, 2026 limekutana na wadau wa usafiri majini mkoani Kigoma kwa lengo la kukusanya maoni kuhusu maombi ya nauli za abiria na mizigo kwa meli ya MV. Liemba, yaliyowasilishwa na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO).
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Nahson Sigalla, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa TASAC, ameeleza kuwa maoni ya wadau ni muhimu katika kuhakikisha kuwa maamuzi kuhusu nauli yanazingatia mahitaji ya watumiaji wa huduma za meli na maslahi ya sekta ya usafiri majini kwa ujumla.
Amesema kuwa mkutano huo umefanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415, kinachotaka TASAC kuwashirikisha wadau kabla ya kuidhinisha viwango vya nauli au tozo.
Bw. Sigalla amefafanua kuwa mkutano huo haukuwa wa kufanya uamuzi wa viwango vya nauli vitakavyotumika, bali ulikuwa jukwaa la kukusanya maoni ya wadau kwa uwazi na kuwapa washiriki fursa sawa ya kutoa mapendekezo yao.
Katika mkutano huo, wadau walipata fursa ya kupokea wasilisho kutoka TASHICO, lilitolewa na Afisa Uendeshaji Mwandamizi, Bw. Baraka Bigambo ambaye ameeleza kuhusu viwango vya nauli vinavyopendekezwa na sababu za maombi hayo.
Mkutano huo ulio washirikisha wasafiri, wafanyabiashara na makampuni ya ugomboaji wa shehena ni sehemu ya mchakato wa kisheria unaopaswa kufuatwa kabla ya TASAC kuidhinisha viwango vipya vya nauli na tozo za huduma za usafiri majini ukiwa na lengo la kuhakikisha kuwa maamuzi kuhusu maombi ya nauli za MV. Liemba yanafanyika kwa kuzingatia matakwa ya sheria na maoni ya wadau wanaotumia huduma za meli hiyo.
Wadau pia walielekezwa kuwa wanaweza kuwasilisha maoni yao kwa maandishi katika ofisi za TASAC zilizopo Kigoma, Rukwa au Dar es Salaam, kabla au ifikapo Oktoba 30, 2026, kwa mujibu wa tangazo la umma lililotolewa Oktoba 14, 2026.