TASAC YAFANYA UKAGUZI WA VYOMBO VYA UVUVI KIGAMBONI
Maafisa wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 21 Agosti, 2026, wamefanya ziara katika maeneo ya wavuvi wilayani Kigamboni, Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua vyombo vya majini na kutoa elimu kuhusu usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira ya bahari.
Zoezi hilo limehusisha uhakiki wa hali ya usajili na leseni za vyombo, tathmini ya uzingatiaji wa matakwa ya usalama wa usafiri majini, pamoja na kubaini vyombo visivyosajiliwa au vinavyoendeshwa bila kuzingatia matakwa ya kisheria. Pia, wamiliki na waendeshaji wa vyombo wamepewa elimu na mwongozo kuhusu taratibu za kiudhibiti.
Katika ziara hiyo, wavuvi wameelimishwa kuhusu umuhimu wa kusajili na kupata leseni za vyombo vyao, kuwa na vifaa muhimu vya usalama na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usafiri wa majini ili kulinda maisha ya watu na mali zao.
Aidha, wamehimizwa kutunza mazingira ya majini kwa kuepuka kutupa taka, mafuta na vitu vingine vinavyoweza kuchafua bahari na kuathiri ikolojia pamoja na uhai wa viumbe wa majini.
Maafisa hao pia wameeleza majukumu yanayotekelezwa na TASAC katika kusimamia na kudhibiti shughuli za usafiri majini, ikiwemo kuhakikisha uzingatiaji wa sheria, kanuni na viwango vinavyohusu usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira ya majini.
Zoezi hilo limeongozwa na Bw. Rahim Dhahiri, akiambatana na maafisa wenzake wanaohusika na Ukaguzi na Usajili wa Vyombo vya Majini kutoka Idara ya Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ya TASAC.
Bw. Dhahiri amesisitiza umuhimu wa wavuvi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha shughuli za uvuvi na usafirishaji majini zinafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vya usalama. Pia, amewahimiza kutoa taarifa wanapobaini changamoto au vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama majini.
Katika ziara hiyo, TASAC imesikiliza maoni, changamoto na mapendekezo ya wavuvi kuhusu shughuli zao za kila siku. Maoni hayo yatasaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Shirika na kuimarisha ushirikiano na wadau kwa ajili ya usafiri wa majini ulio salama, wenye ulinzi na unaozingatia utunzaji wa mazingira.