Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAFANYA KIKAO CHA WADAU KUHUSU UANZISHWAJI WA BANDARI KAVU MKOANI TANGA

Imewekwa: 18 August, 2026
TASAC YAFANYA KIKAO CHA WADAU KUHUSU UANZISHWAJI WA BANDARI KAVU MKOANI TANGA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo, Agosti 17, 2026, limefanya kikao cha wadau wa Serikali ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uanzishwaji, usimamizi na uendeshaji wa bandari kavu mkoani Tanga.

Kikao hicho, kilichofanyika katika Ukumbi wa Bandari House jijini Tanga, kiliwakutanisha wataalamu kutoka TASAC, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na taasisi za Serikali zinazohusika na utoaji wa vibali, leseni na usimamizi wa shughuli za bandari kavu.

Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema uanzishwaji wa bandari kavu ni hatua muhimu katika kuboresha mtiririko wa mizigo na kuiwezesha Bandari ya Tanga kutekeleza kwa ufanisi shughuli zake za msingi za kupakua na kupakia shehena melini.

Ameeleza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeiwezesha Bandari ya Tanga kupokea meli kubwa gatini na kuongeza kiwango cha shehena inayohudumiwa.

Mhe. Balozi Dkt. Burian amezihimiza taasisi zinazohusika kuimarisha zaidi ushirikiano kikamilifu na kuwa mabalozi wazuri wa Bandari ya Tanga ili kuvutia wateja kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, amesema TASAC imewakutanisha wadau hao ili kujadiliana na kuweka uelewa wa pamoja kuhusu taratibu za uanzishwaji wa bandari kavu, utoaji wa vibali na leseni pamoja na usimamizi wa shughuli zake.

Bw. Salum amesema kikao hicho pia kimelenga kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi zinazohusika ili kuhakikisha bandari kavu zinaanzishwa na kuendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vilivyowekwa.

Ameongeza kuwa uendeshaji wenye tija wa bandari kavu utasaidia kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Tanga, kuharakisha uondoshaji wa shehena na kupunguza muda pamoja na gharama kwa wafanyabiashara.

Aidha, kikao hicho kimejadili mchango wa bandari kavu katika kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia shehena, na kuongeza mapato ya Serikali.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo