Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAFANYA KIKAO CHA MASHAURIANO NA WADAU WA HUDUMA BANDARINI

Imewekwa: 25 February, 2026
TASAC YAFANYA KIKAO CHA MASHAURIANO NA WADAU WA HUDUMA BANDARINI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) leo tarehe 24 Februari 2026 limefanya kikao cha mashauriano na wadau wa sekta ya usafiri majini jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujadili na kutoa ufafanuzi kuhusu marekebisho ya kanuni za utoaji wa huduma mbalimbali bandarini.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi, Bw. Nahson Sigalla, amesisitiza kuwa mashauriano ni nguzo muhimu ya udhibiti na ni njia ya kuongeza uelewa na ufanisi katika utoaji wa huduma bandarini.

Bw. Sigalla amesema kuwa TASAC ina jukumu la kuandaa mapendekezo ya kanuni, kutoa leseni, pamoja na miongozo mbalimbali inayosimamia soko la usafiri majini, huku utekelezaji wake ukiwa mikononi mwa wadau wanaotoa huduma bandarini. 

Ameongeza kuwa pale panapofanyika marekebisho ya kanuni au miongozo yaliyotokana na maoni ya wadau na kufikia hatua ya kutekelezwa, ni muhimu kwa TASAC kukutana na wadau hao ili kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma kwenye soko la huduma za usafiri majini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TASAC, Wakili Judith Kakongwe, ameeleza kuwa marekebisho yaliyofanyika yamelenga kupanua wigo wa huduma, kutoa ufafanuzi wa kisheria, na kuimarisha uwazi katika utekelezaji wa kanuni, huku yakilinda maslahi ya Watanzania.

Nae, Mwakilishi wa DP World Dar es Salaam Ltd, Bw. Quilnus Matembo, amewakumbusha watoa huduma bandarini umuhimu wa kuzingatia taratibu za Afya, Usalama na Mazingira, ikiwemo matumizi ya vifaa kinga, ili kulinda maisha yao na mazingira wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Wadau walioshiriki katika kikao hicho wameishukuru TASAC kwa kuendelea kuwawezesha wazawa, kuwajengea uwezo, na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania. Wameeleza kuwa licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali, kazi nyingi za kuhudumia meli bandarini zinaendelea kufanywa na wazawa. 

TASAC imeahidi kuendelea kupokea na kushughulikia changamoto za kiutendaji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ili kuhakikisha sekta ya usafiri majini inaendelea kuimarika na kuchangia katika Uchumi wa taifa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo