TASAC YAENDESHA MAFUNZO KWA MAKARANI WA SENSA YA VYOMBO VYA MAJINI, MAENEO YA UJENGA NA KUKARABATI MELI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), leo tarehe 28 Septemba, 2026 wameendesha mafunzo kwa makarani watakaoshiriki katika Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara.
Mafunzo hayo yamelenga kuwaandaa makarani hao kwa kuwapatia uelewa na ujuzi unaohitajika katika ukusanyaji wa taarifa sahihi, za uhakika na zenye viwango vinavyokubalika wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Nahson Sigalla, ambaye ni Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi, amesema sensa hiyo ni muhimu katika kuisaidia Serikali kupata takwimu sahihi kuhusu idadi, aina, matumizi na maeneo vilipo vyombo vya majini, pamoja na maeneo ua ujenzi na ukarabati wa meli na vyombo vya majini nchini.
Bw. Sigalla amewataka makarani hao kutekeleza zoezi hilo kwa weledi, uadilifu na umakini, huku wakihakikisha taarifa zinazokusanywa ni sahihi, kamili na zinazingatia taratibu na miongozo iliyowekwa ili kuwezesha kuwa na kanzidata sahihi kwa ajili ya mipango na maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini nchini.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamejikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo namna ya kutambua na kuhesabu vyombo vya majini, ukusanyaji wa taarifa za vyombo, matumizi ya zana za kidijitali katika ukusanyaji wa takwimu, pamoja na namna ya kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa zoezi la sensa.
Sensa hiyo inatarajiwa kufanyika katika maeneo yote ya Tanzania Bara kuanzia tarehe 1 hadi 30 Oktoba, 2026 na itahusisha ukusanyaji wa taarifa za vyombo vya majini, wajenzi na wakarabati meli na vyombo vya usafiri majini, kwa lengo la kujenga kanzidata yenye taarifa sahihi itakayosaidia katika mipango, udhibiti na maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini.