Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAENDELEA KUTOA MAFUNZO YA MFUMO WA MARITIME TRANSPORT e-REGULATORY SYSTEM TANGA

Imewekwa: 07 September, 2026
TASAC YAENDELEA KUTOA MAFUNZO YA MFUMO WA MARITIME TRANSPORT e-REGULATORY SYSTEM TANGA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendelea kutoa mafunzo kwa wadau kuhusu matumizi ya mfumo wa ‘Maritime Transport e-Regulatory System (MTRS)’, mfumo wa kidijitali unaolenga kurahisisha na kuboresha utoaji wa huduma za kiudhibiti katika Sekta ya Usafiri wa Majini nchini.

Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 3 Septemba 2026 katika Ukumbi wa Bandari mkoani Tanga, yakilenga kuwawezesha wadau kuelewa na kutumia mfumo huo katika kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na TASAC.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Afisa Mfawidhi wa TASAC Tanga, Bw. Patrick Nungwe, amesema matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za usafiri wa majini ni muhimu katika kuhakikisha huduma zinapatikana kwa haraka, usahihi na ufanisi zaidi.

Amesema maendeleo ya teknolojia yamekuwa sehemu muhimu katika shughuli mbalimbali za kibandari, ikiwemo Uondoshaji na Ugomboaji wa Shehena (Clearing and Forwarding), Utoaji wa Huduma Mbalimbali Bandarini (Miscellaneous Port Services), pamoja na Uwakala wa Meli, hivyo ni muhimu kutumia mifumo ya kidijitali inayoendana na mahitaji ya sasa.

Mfumo wa MTRS umeanzishwa baada ya kuboreshwa kwa mfumo wa awali wa M-BILL, kwa lengo la kurahisisha utoaji wa leseni na vyeti, usajili na malipo ya huduma za kiudhibiti, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa uzingatiaji wa matakwa ya kisheria.

Kupitia MTRS, watoa huduma wataweza kujisajili na kupata huduma kwa njia ya kidijitali bila kulazimika kufika katika ofisi za TASAC kwa kila hatua ya mchakato, hivyo kupunguza muda na kuongeza ufanisi na uwazi.

Mafunzo hayo yamewakutanisha Mawakala wa Meli, Mawakala wa Forodha na Usafirishaji wa Mizigo (CFA), Watoa Huduma Mbalimbali za Bandari (MPS), Waunganishaji wa Mizigo (Consolidators), pamoja na watoa huduma katika maeneo ya mipakani ya Holili, Namanga na Horohoro.

TASAC imesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau katika matumizi ya mfumo huo ili kuhakikisha huduma za kiudhibiti zinaendelea kutolewa kwa ufanisi, uwazi, weledi na kuendana na maendeleo ya teknolojia.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo