Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC, TEMEKE WAKUTANA KUJADILI MPANGO WA KUENDELEZA KATA 10 ZA MANISPAA YA TEMEKE

Imewekwa: 27 September, 2026
TASAC, TEMEKE WAKUTANA KUJADILI MPANGO WA KUENDELEZA KATA 10 ZA MANISPAA YA TEMEKE

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), tarehe 25 Septemba 2026, lilifanya kikao cha pamoja na Mstahiki Meya, Wabunge kutoka Manispaa ya Temeke, Mkurugenzi pamoja na Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kujadili mpango wa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbqlimbali zikiwemo za Bandari Kavu katika manispaa hiyo.

Ujumbe wa Manispaa ya Temeke uliongozwa na Meya wa Manispaa hiyo, Mstahiki Uzairu Athumani, pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa, Bw. Jomaary Satura, na ulipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, katika Ofisi za TASAC jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimefanyika kufuatia mpango wa kutenga maeneo katika kata mbalimbali za Temeke. TASAC, kwa kuzingatia jukumu lake la kudhibiti uanzishwaji na uendeshaji wa Bandari Kavu nchini, iliratibu kikao hicho kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja na kuweka msingi wa ushirikiano miongoni mwa wadau.

Washiriki walijadili maeneo yaliyopangwa, namna ya utekelezaji wa mpango huo,  pamoja na umuhimu wa kuwashirikisha wananchi wa maeneo yaliyopendekezwa. Kata zinazohusisha katika mpango huo ni; Azimio, Buza, Sandari, Kilakala, Mtoni, Makangarawe, Temeke, Miburani na Yombo Vituka, pamoja na maeneo mahsusi ndani ya kata hizo.

Aidha, Tandika, Chang’ombe na Kurasini hazijajumuishwa katika mpango huo kwa kuwa tayari zimeainishwa katika mipango mingine ya kimkakati. Tandika ni kitovu cha biashara, Chang’ombe ni eneo la viwanda, huku Kurasini likiwa eneo la shughuli za bandari.

Mpango huo umezingatia uwepo wa miundombinu ya barabara, reli ya TAZARA, maeneo ya maegesho pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi zinazohusiana na usafirishaji na biashara. Katika awamu ya kwanza, Keko, Sandari, Kilakala, Mtoni na Azimio zimeainishwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayoendelezwa.

Kikao pia kilijadili utaratibu wa tozo ya kufidia (recovery) gharama za uharibifu wa miundombinu unaochangiwa  na shughuli za Bandari .

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za TASAC na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kujenga uelewa wa pamoja na kuweka msingi wa ushirikiano katika utekelezaji wa mpango huo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo