TASAC NA BEFORWARD JAPAN WAJADILI KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRISHAJI WA MAGARI KUTOKA BANDARINI
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, amekutana na ujumbe kutoka kampuni ya Beforward Japan kujadili mikakati ya kuboresha usafirishaji wa magari yanayoingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam, kwa lengo la kuimarisha usalama wa magari na kulinda ubora wake hadi yanapowafikia wanunuzi.
Katika kikao hicho, pande hizo mbili zilijadili changamoto mbalimbali zinazowakabili Beforward Japan pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuimarisha uwajibikaji katika mnyororo mzima wa usafirishaji.
Beforward Japan ilieleza kuwa huingiza nchini kati ya magari 9,000 hadi 10,000 kila mwezi, hali inayoiweka miongoni mwa waagizaji wakubwa wa magari nchini. Kutokana na idadi hiyo, kampuni ilisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mfumo madhubuti wa usafirishaji unaohakikisha magari yanasafirishwa kwa usalama, bila kupoteza vifaa na bila kuathiri ubora wake.
Majadiliano hayo pia yaligusia umuhimu wa kurahisisha mnyororo wa usafirishaji wa magari kutoka bandarini hadi ICDs ili kupunguza ucheleweshaji, kuongeza uwajibikaji wa wadau wanaohusika na kuhakikisha magari yanawasilishwa kwa wateja yakiwa katika hali ileile yalivyopokelewa bandarini.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Salum amelekeza Shirika kuandaa taarifa rasmi kwa umma (Public Notice) itakayotoa mwongozo kwa wadau kuhusu hatua zinazochukuliwa kuimarisha usalama wa magari na kuboresha utoaji wa huduma katika mnyororo wa usafirishaji.
Kwa upande wake, Bw. Kojiro Matsumura kutoka Beforward Japan ameiomba TASAC kuzingatia ombi la kuitambua kampuni ya Alistair kama Mtoa Huduma za Baharini (Marine Service Provider – MSP) wake, hatua ambayo itaongeza uratibu na ufanisi katika usafirishaji wa magari kutoka bandarini hadi maeneo ya kuhifadhi.
Kufuatia ombi hilo, Bw. Salum ameielekeza kampuni ya Alistair kuwasilisha maombi ya kupata leseni kwa mujibu wa taratibu za TASAC ili iweze kutekeleza shughuli zake kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na kiudhibiti.
TASAC imeeleza itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote wa sekta ya usafirishaji ili kuimarisha usalama wa magari, kuongeza ufanisi wa huduma na kuhakikisha mnyororo wa usafirishaji unakuwa wa kuaminika kwa manufaa ya wafanyabiashara na wananchi.