TANZANIA YAENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIKANDA KATIKA ULINZI NA USALAMA BAHARINI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limeratibu kikao cha wadau kinachojadili ushiriki wa Tanzania katika Vituo vya Kikanda katika Uunganishaji wa Taarifa za Baharini (RMIFC) na Uratibu wa Operesheni (RCOC), pamoja na mchakato wa kuridhia mikataba ya kimataifa, na kuimarisha utendaji wa Kituo cha Kitaifa cha Uratibu wa Operesheni za Pamoja (NJOC).
Kikao hicho cha siku mbili, kilichoanza tarehe Agosti 20 hadi 21, 2026, na kufanyika katika Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Ukoaji (MRCC) jijini Dar es Salaam, kimewakutanisha wadau kutoka taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya ulinzi, usalama na shughuli za baharini.
Kikao kimeongozwa na Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Uchukuzi, Bi. Stella Katondo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikao hicho.
Katika siku ya kwanza, washiriki wamepata uelewa kuhusu majukumu na utendaji wa NJOC na kufanya tathmini ya utekelezaji wake. Majadiliano yamejikita katika namna kituo hicho kinavyoweza kuimarisha uratibu, mawasiliano na ushirikiano baina ya taasisi zinazohusika na masuala ya ulinzi na usalama baharini.
Aidha, washiriki wamepata wasilisho kuhusu NJOC na kufanya ziara katika Kituo cha Uratibu wa Utafutaji na Uokoaji Baharini (MRCC), pamoja na NJOC. Ziara hiyo imelenga kuwajengea wadau uelewa wa kiutendaji kuhusu mifumo na taratibu zinazotumika katika kuratibu shughuli za ulinzi, usalama, utafutaji na uokoaji baharini.
Katika siku ya pili, washiriki wamejadili mpango wa kuimarisha utendaji wa NJOC na umuhimu wa Tanzania kushiriki katika vituo vya kikanda vya RMIFC na RCOC. Pia, wataandaa ramani ya utekelezaji ya kuimarisha kituo hicho na kuweka mikakati ya kuboresha mawasiliano, ushirikiano na uratibu miongoni mwa taasisi husika.
Kikao hicho kinatarajiwa kutoa mapendekezo na hatua madhubuti zitakazoongeza ufanisi wa NJOC na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika mifumo ya kikanda ya kubadilishana taarifa na kuratibu operesheni za baharini.
Hatua hizo zitaiwezesha Tanzania kukabiliana kwa ufanisi zaidi na changamoto za kiusalama baharini, kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kikanda, pamoja na kulinda maslahi ya nchi katika maeneo yake ya baharini.