TAHADHARI YA EL NINO: TASAC YAWAASA WADAU WA USAFIRI MAJINI MKOA WA MARA
Wadau wa usafiri majini katika Mkoa wa Mara wameaswa kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali ya hewa ya El Niño inayotarajiwa kuathiri msimu wa mvua za Vuli 2026, kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Wito huo umetolewa na Afisa Mfawidhi (OIC) wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Mara na Simiyu, Naho. Hezron Lusangija, wakati wa semina ya utoaji elimu kuhusu tahadhari na hatua za kuchukua kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na hali hiyo ya hewa katika mialo mbalimbali ya Mkoa wa Mara.
Naho. Lusangija amesema kuwa, katika kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, ni wajibu wa kila mmiliki na mtumiaji wa chombo cha usafiri majini kuhakikisha chombo kinakuwa katika hali salama na kina vifaa vyote muhimu vya usalama kabla ya kuanza safari, hususan jaketi okozi, pamoja na kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika ipasavyo.
“Ni muhimu kwa kila anayefanya kazi katika chombo kuhakikisha chombo kimesajiliwa na TASAC na kina cheti halali ambacho hakijaisha muda wake. Vilevile, chombo kiwe na jaketi okozi za kutosha na watumiaji wazivae wakati wote wanapokuwa safarini,” alisema Naho. Lusangija.
Aidha, amewataka wadau wa usafiri majini kuendelea kuzingatia taratibu na kanuni za usalama wa usafiri majini, ikiwemo kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka husika kabla na wakati wa safari.
TASAC inaendelea kuwaasa wananchi na wadau wote wa usafiri majini kuchukua tahadhari, kuzingatia maelekezo ya usalama na kuepuka kusafiri endapo hali ya hewa si salama, ili kulinda maisha ya abiria, wasafiri na watumiaji wengine wa vyombo vya usafiri majini.