NAIBU SPIKA SILLO ATEMBELEA BANDA LA TASAC KATIKA MEL WEEK, ARUSHA
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Baran Sillo (Mb.), ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano la Tano la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (Monitoring, Evaluation and Learning – MEL Week), leo tarehe 23 Septemba 2026, ametembelea Banda la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), katika Hoteli ya Ngurdoto Mountain, Arusha, na kupata fursa ya kufahamu kwa kina majukumu na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika.
Akiwa katika banda hilo, Mhe. Sillo ameelezwa kuhusu majukumu ya TASAC katika kusimamia na kudhibiti shughuli za wakala wa meli, pamoja na utekelezaji wa majukumu yake kwa kuzingatia weledi, ufanisi na uwajibikaji.
Maelezo hayo yametolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Shirika, Bw. Hamid Mbegu, ambaye amemweleza Mhe. Naibu Spika kuhusu maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya TASAC, pamoja na namna Shirika linavyotumia mifumo ya ufuatiliaji, tathmini na kujifunza katika kuboresha utendaji na utoaji wa huduma.
Aidha, katika kongamano hilo, TASAC imetunukiwa Tuzo ya Ubora katika Ushirikiano (Excellence in Partnership Award), ikiwa ni utambuzi wa mchango wa Shirika katika kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa shughuli zinazolenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na ujifunzaji.
Kongamano la Tano la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza limeanza tarehe 22 Septemba 2026 na linatarajiwa kuhitimishwa tarehe 26 Septemba 2026. Kongamano hilo linawakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu za kuimarisha matumizi ya ushahidi katika kuboresha utekelezaji wa programu na shughuli za maendeleo.