NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA UCHUKUZI, BW. ABDALLAH MITAWI, AFANYA ZIARA TASAC
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Abdallah Mitawi, leo Agosti 26, 2026, amefanya ziara katika Makao Makuu ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujitambulisha, kufahamiana na Menejimenti pamoja na kupata uelewa kuhusu majukumu na shughuli za Shirika.
Akizungumza na Menejimenti, Bw. Mitawi ameipongeza TASAC kwa kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuimarisha gawio linalowasilishwa Serikalini. Amesema mafanikio hayo yanaonesha uwajibikaji, usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na kuzingatiwa kwa misingi ya utawala bora.
Aidha, ameipongeza TASAC kwa kusimamia sekta muhimu ya usafiri majini, ambayo husafirisha takribani asilimia 90 ya shehena za biashara duniani. Ameeleza kuwa usimamizi madhubuti wa sekta hiyo ni muhimu katika kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Bw. Mitawi ameitaka TASAC kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu. Amesisitiza kuwa mipango, mikakati na bajeti za Shirika zinapaswa kuandaliwa kwa kuongozwa na Mpango huo ili kuchangia kikamilifu katika kufikiwa kwa malengo ya Taifa.
Ameelekeza TASAC kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa bima ya mizigo ili kulinda maslahi ya wafanyabiashara, wamiliki wa mizigo na uchumi wa Taifa. Pia, amelitaka Shirika kuimarisha udhibiti wa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na mafuta baharini (Oil Pollution) kupitia usimamizi madhubuti wa meli, bandari na shughuli nyingine za usafiri majini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, ametoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Shirika pamoja na mafanikio yaliyofikiwa. Miongoni mwa mafanikio hayo ni ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha Uratibu wa Utafutaji na Uokozi Majini (MRCC), kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato na gawio linalowasilishwa Serikalini.
Bw. Salum ameahidi kuwa TASAC itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali na kusimamia sekta ya usafiri majini kwa ufanisi ili kuimarisha sekta ya usalama ya usafiri kwa njia ya maji.