MTENDAJI MKUU OSHA AVUTIWA NA HUDUMA ZA TASAC KATIKA TAMASHA LA KIZIMKAZI 2026
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, ametembelea Banda la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) katika Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi na kuvutiwa na kazi inayofanywa na Shirika hilo katika kusimamia huduma ya Usafirishaji Majini kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Akiwa katika Bandani hapo leo, Agosti 13, 2026, katika Viwanja vya Maonesho Dimbani Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Bi. Mwenda amepata maelezo kuhusu majukumu na huduma mbalimbali zinazotolewa na TASAC, ikiwemo usimamizi wa usalama wa vyombo vya usafiri majini pamoja na utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vifaa okozi.
Baada ya kupata maelezo hayo, Bi. Mwenda ameipongeza TASAC kwa kazi nzuri inayofanya katika kutekeleza majukumu yake, hususan juhudi za kuhakikisha usalama unaendelea kupewa kipaumbele katika shughuli za usafiri majini kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Ziara hiyo ya Bi. Mwenda imetoa nafasi ya kubadilishana uelewa kuhusu umuhimu wa taasisi za Serikali kuendelea kushirikiana katika kuimarisha masuala ya usalama na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
TASAC inaendelea kushiriki Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi kwa kutoa elimu kuhusu majukumu na huduma zake, huku ikiwahamasisha wananchi na wadau kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama katika usafiri kwa njia ya maji.