Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MKURUGENZI MKUU TASAC AWASHUKURU WADAU WA MAONESHO YA SABASABA

Imewekwa: 10 July, 2026
MKURUGENZI MKUU TASAC AWASHUKURU WADAU WA MAONESHO YA SABASABA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, amewashukuru wadau na wananchi wanaoendelea kutembelea banda la TASAC katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Bw. Salum ametoa shukrani hizo leo, Julai 5, 2026, alipotembelea banda la shirika hilo na kujionea ushiriki wa wadau pamoja na mwitikio wa wananchi wanaofika kupata elimu kuhusu shughuli na huduma zinazotolewa na TASAC.

“Nawashukuru wadau wote wanaotembelea banda la TASAC katika maonesho haya. Ninatoa wito kwa wananchi na wadau wote kufika hapa kujifunza masuala mbalimbali kuhusu TASAC, ikiwemo fursa zilizopo katika sekta ya uchukuzi kwa njia ya maji,” amesema Bw. Salum.

Amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kuelimisha umma kuhusu majukumu ya TASAC katika kusimamia usalama, ulinzi na ubora wa huduma za usafiri majini, sambamba na kuhamasisha uwekezaji na matumizi ya fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yalianza Juni 28, 2026, na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026, yakihusisha taasisi za umma na binafsi kutoka ndani na nje ya nchi zikionesha bidhaa, huduma na teknolojia mbalimbali.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo