MKURUGENZI MKUU TASAC AFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA MKOA WA TANGA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed M. Salum, leo Agosti 17, 2026, amefanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Mazungumzo hayo yamejikita katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya usafiri majini, hususan uanzishwaji, usimamizi na uendeshaji wa bandari kavu mkoani Tanga.
Viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya TASAC, Serikali ya Mkoa na wadau wengine ili kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuhakikisha bandari kavu inaanzishwa na kuendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Bw. Salum ameeleza kuwa TASAC itaendelea kutekeleza majukumu yake ya udhibiti na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau, ili kuhakikisha huduma za bandari kavu zinakuwa salama, zenye ufanisi na ushindani.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Dkt. Burian amesema Serikali ya Mkoa wa Tanga ipo tayari kushirikiana na TASAC pamoja na taasisi nyingine katika kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya Bandari kavu mkoani Tanga.
Amesisitiza kuwa kuanzishwa kwa bandari kavu kutasaidia kurahisisha mtiririko wa mizigo, kupunguza msongamano bandarini na kuiwezesha Bandari ya Tanga kutekeleza kwa ufanisi zaidi shughuli zake za msingi za kupakua na kupakia shehena melini.
Mazungumzo hayo yamefanyika ikiwa ni sehemu ya juhudi za TASAC za kushirikisha viongozi na wadau katika kuendeleza sekta ya usafiri majini na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi mkoani Tanga na Taifa kwa ujumla.