Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MHE. KIHENZILE: SERIKALI YAIPA KIPAUMBELE SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Imewekwa: 25 September, 2026
MHE. KIHENZILE: SERIKALI YAIPA KIPAUMBELE SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema Serikali itaendeleagʻ kuwekeza katika sekta ya usafiri majini kwa lengo la kuongeza ufanisi, usalama, ushindani na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Mhe. Kihenzile ameyasema hayo leo, Septemba 24, 2026, jijini Tanga wakati akifunga rasmi Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani 2026, yenye kaulimbiu “Kutoka Sera hadi Utekelezaji: Kuimarisha Ubora Katika Sekta ya Usafiri Majini.”

Amesema Tanzania ina nafasi ya kimkakati katika usafiri majini kutokana na kuwa mwambao wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu, huku bandari zake zikiwa lango la biashara kwa Tanzania na nchi jirani zisizo na bandari.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya bandari, usalama wa vyombo, huduma za mizigo na abiria, matumizi ya teknolojia ⁷na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya IMO.

Mhe. Kihenzile amewataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo kuhakikisha vinakidhi viwango vya usalama, vinakaguliwa na kuwa na leseni pamoja na vifaa vya kuokoa maisha. Pia amezitaka Wizara, TASAC na ZMA kujiandaa kukabiliana na athari za mvua kubwa zinazotarajiwa katika msimu wa Vuli 2026.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, amewataka wadau kutafsiri sera, sheria, viwango na mikataba ya kimataifa kwa vitendo ili kuimarisha usalama, ufanisi na ubora wa huduma.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta hiyo, ikiwemo kuboresha bandari, kuendeleza mafunzo ya mabaharia na kuimarisha mifumo ya kidijitali. Amesema hadi Machi 2026, TASAC ilitoa vyeti 15,948 vya mabaharia, ikilinganishwa na 10,270 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 55.29.

Bw. Salum amesema Tanzania pia imekamilisha Kituo cha Kikanda cha Utafutaji na Uokoaji Mwanza na inaendelea na ununuzi wa boti za utafutaji na uokoaji, huku TASAC ikiandaa ununuzi wa boti maalum za kukabiliana na uchafuzi wa mafuta baharini.

Kuhusu El Niño, amesema TASAC inaendelea na kampeni ya uhamasishaji iliyofikia zaidi ya mikoa minane, bandari sita na vivuko vitatu, pamoja na mialo na vivuko 16.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo