MHE. KIHENZILE ASISITIZA USHIRIKIANO WA TANZANIA NA ZAMBIA SEKTA YA UCHUKUZI
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amezindua mashine ya reach stacker ya kampuni ya Zambia Cargo and Logistics Limited (ZCL) katika Depo ya Mukuba, Dar es Salaam, na kusisitiza kuimarika kwa ushirikiano wa Tanzania na Zambia katika sekta ya uchukuzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kihenzile ameipongeza ZCL kwa kuongeza shehena kutoka makontena 15,649 kwa mwaka 2021 hadi kufikia makontena zaidi ya 40,000 kwa mwaka 2025 ambayo ni ishara ya ufanisi na uwekezaji madhubuti katika Miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam.
Mhe. Kihenzile ameongeza kuwa Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu ya bandari, reli, barabara na mipaka ili kuboresha biashara kikanda, ikiwamo ujenzi wa SGR, maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam na upanuzi wa Bandari ya Mtwara.
Aidha, ameiomba Zambia kuharakisha ufunguzi wa Nakonde One Stop Border Post ili kupunguza msongamano wa magari Tunduma–Nakonde.
Katika hafla hiyo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Sylvester Kanyika ameeleza kuwa uwekezaji huo unahakikisha mnyororo wa usafirishaji mizigo ya Zambia kupitia Dar es Salaam unakuwa thabiti na salama zaidi.
Bw. Kanyika ameongeza kuwa TASAC kuwa itaendelea kushirikiana na wadau katika sekta ya usafirishaji majini katika kuhakikisha taratibu za kisheria, usalama wa majini na ubora wa huduma vinafuatwa ipasavyo.