MAONESHO YA UTAFUTAJI NA UOKOAJI YAONESHA UTAYARI WA TANZANIA KATIKA UTAFUTAJI NA UOKOAJI
Maonesho ya utafutaji na uokoaji baharini yaliyofanyika tarehe 23 Septemba 2026 katika Raskazone Swimming Club, Tanga, yameonesha utayari wa Tanzania katika kukabiliana na dharura na kuokoa maisha ya watu wanaotumia usafiri wa majini.
Maonesho hayo, yaliyofanyika ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Usafiri kwa Njia ya Maji Duniani 2026, ambapo yalihusisha zoezi la kuokoa maisha katika tukio la hatari linalowalazimu mabaharia kuachana na meli (abandon ship drill). Katika zoezi hilo, Nahodha wa jahazi alitoa amri ya kuondoka kwenye chombo, na boti ya utafutaji na uokoaji ya TASAC ilitekeleza zoezi la uokoaji.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Mgeni Rasmi, Nahodha Mussa Mandia, amesema zoezi hilo limeonesha kwa vitendo utekelezaji wa kaulimbiu ya IMO ya mwaka 2026 na 2027, “Kutoka Sera hadi Utekelezaji: Kuimarisha Ubora katika Sekta ya Usafiri Majini”.
Nahodha Mandia alisema Tanzania imeendelea kuwekeza katika usalama majini, ikiwa na boti nne za utafutaji na uokoaji, moja Tanga, moja Kigoma na mbili Mwanza, pamoja na boti ya huduma za wagonjwa Mwanza na boti nne za doria Dar es Salaam.
Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuboresha miundombinu ya usafiri na uchumi wa bahari, akisema maboresho ya Bandari ya Tanga, ikiwemo magati na miundombinu ya kuhudumia meli, yameongeza uwezo wa bandari.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira wa Wizara ya Uchukuzi, Bi. Stella Katondo, amesema maonesho hayo ni muhimu katika kujenga utayari wa wadau na kuongeza uelewa wa namna ya kukabiliana na dharura baharini.
Amesema usalama wa abiria na wahudumu unahitaji ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za usalama, waendeshaji wa vyombo na wananchi, huku akizipongeza TASAC na ZMA kwa kuratibu maadhimisho hayo na kuendelea kusimamia usalama wa usafiri wa majini nchini.