Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

KATIBU TAWALA KIGOMA AIPONGEZA TASAC KWA KUENDELEA KUSIMAMIA VIZURI KUIMARISHA SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Imewekwa: 10 July, 2026
KATIBU TAWALA KIGOMA AIPONGEZA TASAC KWA KUENDELEA KUSIMAMIA VIZURI KUIMARISHA SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Ndugu Hassan Rugwa, leo tarehe 05 Julai, 2026, ametembelea banda la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya SabaSaba yanayoendelea katika viwanja vya SabaSaba jijini Dar es Salaam.

 

Akiwa katika banda hilo, Ndugu Rugwa alipata maelezo kuhusu majukumu ya TASAC katika kusimamia usalama wa vyombo vya usafiri majini, kutoa huduma za usajili na ukaguzi wa vyombo vya majini, kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na kanuni za usafiri wa majini, pamoja na kulinda mazingira ya majini dhidi ya uchafuzi wa mazingira ya bahari unaoweza kusababishwa na shughuli za usafiri na usafirishaji majini.

 

Baada ya kutembelea banda hilo, Ndugu Rugwa ameipongeza TASAC kwa namna inavyotekeleza majukumu yake ya Usimamizi wa Seka ya Usafiri majini kwa weledi na kujituma, akieleza kuwa kazi zinazofanywa na Shirika hilo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa usafiri kwa njia ya maji nchini.

 

Amesema juhudi hizo zimechangia kupunguza ajali za majini, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi salama ya vyombo vya usafiri majini, pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali za kulinda maisha ya wananchi na kuhifadhi mazingira ya majini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa TASAC kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia maonesho kama ya SabaSaba ili wananchi na wadau  wa sekta ya usafiri majini wapate fursa ya kufahamu huduma na majukumu yanayotekelezwa na Shirika hilo na wajibu wao katika kuhakikisha usalama wa usafiri kwa njia ya maji.

 

Aidha, ameishauri TASAC kutoa Elimu zaidi kwa Wananchi wanaoingiza bidhaa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na makampuni ya uondoshaji shehena bandarini kuhusu umuhimu wa kutoa mizigo bandarini kwa wakati ili kupunguza idadi ya mizigo inayohifadhiwa katika bandari kavu.

 

Pia ameshauri makampuni ya kuondosha shehena waelimishwe umuhimu wa kufanya majukumu yao katika bandari kavu za mikoani kama vile Morogoro, Pwani na Dodoma ili kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo