KAMATI YA MAADHIMISHO YA SIKU YA USAFIRI MAJINI DUNIANI YATOA JAKETI OKOZI KWA WADAU TANGA
Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani, ikiongozwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), imetoa jaketi okozi kwa wadau wa usafiri majini mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha uzingatiaji wa usalama katika shughuli za usafiri majini.
Utoaji wa jaketi hizo umefanyika leo tarehe 22 Septemba, 2026 katika Bandari ya Tanga, wakati wa zoezi la kutoa elimu kwa wadau wa usafiri majini kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani kinachotarajiwa kufanyika Septemba 24, 2026.
Akizungumza katika tukio hilo, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Maandalizi, Nahodha Tumba Said Tumba, amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya jaketi okozi, akieleza kuwa uvaaji wake ni hatua muhimu katika kujikinga na kujiokoa endapo kutatokea dharura wakati wa safari au shughuli nyingine za majini.
“Uvaaji wa jaketi okozi ni muhimu kwa usalama wa mtu anapokuwa katika shughuli za majini, kwani humsaidia kujiokoa endapo chombo kitakumbwa na dharura,” alisema Nahodha Tumba.
Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Tanga, Nahodha David Chiragi, amesema TASAC itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za usalama wa usafiri majini, ikiwemo kuhakikisha watumiaji wa vyombo vya majini wanazingatia matakwa ya matumizi ya jaketi okozi.
Amesema Shirika litaendelea kuchukua hatua stahiki kwa watu watakaokiuka matakwa ya sheria na kanuni za usalama, ikiwemo kutovaa jaketi okozi wakati wanapokuwa katika shughuli za usafiri majini.
Aidha, Nahodha Chiragi amesema utoaji wa elimu kwa wadau ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani, ambayo hutoa fursa ya kuwakumbusha wadau na wananchi kwa ujumla umuhimu wa kuzingatia usalama katika shughuli za usafiri na usafirishaji majini.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa miongoni mwa wadau kuhusu umuhimu wa usalama majini, pamoja na kujenga utamaduni wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama wakati wote wanapokuwa katika shughuli za majini.