JWTZ YAFANYA ZIARA YA MAFUNZO MRCC - TASAC
Shirika la Uwakala Meli Tanzania (TASAC) limepokea ugeni wa wanafunzi kutoka Shule ya Kijeshi ya Ubaharia (JWTZ) Kamandi ya Wanamaji kutoka Kigamboni, Dar es Salaam, tarehe 19/10/2026 kwenye ofisi za Kituo cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji majini (MRCC – TASAC) jijini Dar Es salaam.
Ugeni huo umetembelea Kituo cha kuratibu Shughuli za Utafutaji na Uokoaji majini kilichopo Dar es salaam pamoja na Kituo cha Kitaifa cha Uratibu wa Pamoja wa Ulinzi na Usalama Baharini (NJOC) kwa lengo la kujifunza kwa vitendo.
Afisa Mkaguzi wa Vyombo vya Usafiri Majini Nahodha. Awadhi Musa amewashukuru wanafunzi hao kwa kuichagua TASAC kuja kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo jinsi Kituo cha Kuratibu Shughuli za Utafutaji na Uokoaji cha Dar es salaam kinavyohudumia wananchi.
" Tunashukuru kuja kwenu na naomba tuendelee kushirikiana kwenye majukumu ya kuwahudumia wananchi kwa usafiri salama na bora", amesema Bw. Musa.
Aidha, Luteni Kamanda Nicholous Mwakajegela kiongozi wa msafara kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ameishukuru TASAC kwa kuendelea kuweka milango wazi na kushirikiana katika kudhibiti matumizi mazuri ya maeneo ya maji yetu.
"Tumeichagua TASAC na kuwaleta Maafisa na Askari wanafunzi katika Shule ya Kijeshi ya Ubaharia kuja kujifunza vema jinsi Shirika hili linavyotekeleza majukumu ya utafutaji na kuratibu uokoaji majini pale ajali inapotokea". Amesema Mwakajegela.
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na TASAC wameendelea kujenga mahusiano ya karibu ya kupashana habari na uzoefu. Maafisa na Askari hao wamejifunza masuala mengi na kuona kumbe raia wanaweza kuwasaidia kuwapa taarifa zitakazosaidia kulinda rasilimali za nchi.
Ugeni huo umetembelea Kituo cha kuratibu Shughuli za Utafutaji na Uokoaji majini kilichopo Dar es salaam pamoja na Kituo cha Kitaifa cha Uratibu wa Pamoja wa Ulinzi na Usalama Baharini (NJOC) na kupata wasaa wa kujifunza kwa vitendo.
Naye Luteni Kamanda Robert Leonard ameeleza namna mifumo ya kituo hicho inavyotumika kutoa taarifa na kuratibu wadau katika kushiriki zoezi la utafutaji na uokoaji pindi inapotokea dharura majini.
“Mifumo yetu ina muingiliano na wadau wa utafutaji na uokoaji kulingana na dharura inayotokea majini na ina uwezo wa kutambua uelekeo wa chombo na mahali kilipo kiwapo safarini na kurahisisha kutoa usaidizi mara dharura inapotokea,” amesema Luteni Kamanda Leonard.
Ugeni huo pia ulipata fursa ya kupata maelezo ya kina kuhusu utaratibu unaotumika kupokea taarifa zinazosaidia kuratibu zoezi la uokoaji, utoaji taarifa ya hali ya hewa majini pamoja na matumizi ya rada katika kutoa taarifa kwa mfumo wa GPS ili kusaidia kutoa uelekeo wa masafa na mawasiliano ya satelaiti kwa meli zinazofanya safari ndani na nje ya Tanzania ikiwemo “Distress” na “Navigation Warning”.