Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WADAU WA SEKTA YA UCHUKUZI WAHIMIZWA KUIMARISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA NA USHIRIKIANO KUFIKIA DIRA YA TAIFA 2050

Imewekwa: 18 November, 2026
WADAU WA SEKTA YA UCHUKUZI WAHIMIZWA KUIMARISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA NA USHIRIKIANO KUFIKIA DIRA YA TAIFA 2050

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb.), amewahimiza wadau wa sekta ya uchukuzi kuimarisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) pamoja na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuharakisha utoaji wa huduma za uchukuzi fungamanishi na kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa 19 wa Wadau wa Sekta ya Uchukuzi na Tathmini ya Utendaji wa Sekta hiyo, uliofanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza tarehe 17 Novemba 2026, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Mkama amesema mafanikio ya uwekezaji katika sekta hiyo yanapaswa kupimwa kwa mchango wake katika kupunguza gharama za usafiri, muda wa safari, kurahisisha biashara, kuimarisha usalama na kuongeza tija kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa maazimio ya mkutano huo unapaswa kuleta matokeo yanayoonekana katika kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza fursa za kiuchumi ndani na nje ya nchi, akibainisha kuwa teknolojia na ushirikiano ni nyenzo muhimu katika kufikia malengo hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Hamid Mbegu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, amesema TASAC itaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika usimamizi wa usalama wa usafiri majini, utunzaji wa mazingira na udhibiti wa huduma za usafiri majini.

Ameeleza kuwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA imeongeza ufanisi katika utoaji wa leseni, usajili wa mabaharia na ukaguzi wa vyombo vya majini, huku mfumo wa e-Mrejesho ukiimarisha mawasiliano kati ya Shirika na wadau wake.

Naye, Meneja wa Ufuatiliaji na Tathmini wa TASAC, Bw. Makiri Ngangaji, amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Shirika limefikia asilimia 100 ya uzingatiaji wa masharti katika vituo vya bandari vilivyofuatiliwa na kutoa jumla ya vyeti 26,734 kwa mabaharia. Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji katika teknolojia, mafunzo ya wataalamu na kuimarisha mifumo ya usimamizi.

Mkutano huo wa siku mbili umefanyika chini ya kaulimbiu: “Kuharakisha Utoaji wa Huduma za Uchukuzi Fungamanishi, Ufadhili Endelevu na Uwajibikaji wa Sekta kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” ukishirikisha wadau wa Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo