Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

VIJANA WAASWA KUTAMBUA MABADILIKO YA SOKO LA AJIRA

Imewekwa: 12 October, 2026
VIJANA WAASWA KUTAMBUA MABADILIKO YA SOKO LA AJIRA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, amewataka vijana kujiandaa na mabadiliko ya soko la ajira kwa kujifunza ujuzi unaohitajika, kujiajiri na kutumia fursa zilizopo kukuza biashara zao.

Wito huo umetolewa leo, Oktoba 10, 2026, wakati akizindua rasmi Maonesho ya Wiki ya Vijana kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Prof. Mkenda amesema kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 nchini kimepungua kutoka asilimia 8.3 mwaka 2024 hadi asilimia 7.5 mwaka 2025, lakini bado juhudi zinahitajika kuongeza ajira zenye tija na staha.

“Hatua hii ni chanya, lakini haimaanishi kuwa changamoto ya ajira imekwisha. Tunapaswa kuongeza kasi ya uzalishaji wa ajira, kuimarisha ujuzi unaohitajika sokoni na kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kujiajiri na kukuza biashara zao,” amesema.

Ameongeza kuwa maendeleo ya teknolojia, akili unde (AI), biashara mtandao, nishati safi, uchumi wa buluu, kilimo cha kisasa na huduma za kidijitali yanabadilisha aina za kazi na ujuzi unaohitajika, hivyo vijana wanapaswa kujiandaa kwa mahitaji ya uchumi wa sasa na baadaye.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Mawasiliano Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bi. Mariam Mwayela, amewahimiza vijana wa Rukwa na Tanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa za ajira na biashara katika sekta ya usafiri majini.

Bi. Mwayela amesema sekta hiyo ina fursa mbalimbali, zikiwemo kazi za manahodha, maofisa wa meli, wahandisi wa meli, mabaharia, wahudumu wa vyombo vya majini, mawakala wa meli pamoja na wapishi.

Ameeleza kuwa TASAC inashiriki maonesho hayo kutoa elimu kwa vijana kuhusu fursa za ajira, taaluma na biashara katika sekta ya usafiri majini.

Maonesho ya Wiki ya Vijana yanafanyika sambamba na shughuli za kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani Rukwa kuanzia Oktoba 8 hadi 14, 2026.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo