Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MHE. KIHENZILE: TASAC IENDELEE KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRI MAJINI NA KUVUTIA WAWEKEZAJI

Imewekwa: 10 July, 2026
MHE. KIHENZILE: TASAC IENDELEE KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRI MAJINI NA KUVUTIA WAWEKEZAJI

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amelielekeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuendelea kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa sheria na kanuni za usafiri majini, huku likiimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji yatakayowavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika sekta ya usafiri wa majini.

 

Mhe. Kihenzile ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, leo Julai 6, 2026 alipokuwa akitembelea Banda la TASAC katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

 

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo na kujionea huduma zinazotolewa na Shirika, Mhe. Kihenzile amesema pamoja na jukumu lake la udhibiti, TASAC inapaswa kuwa chachu ya kukuza uwekezaji kwa kuhakikisha sekta ya usafiri wa majini inaendelea kuwa salama, yenye uhakika na inayozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

 

"Tunataka kila atakayeleta meli, boti au chombo kingine cha majini nchini awe na uhakika kuwa uwekezaji wake uko salama. Serikali imejipanga kulinda wawekezaji na mitaji yao ili waendelee kuzalisha ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi. Haya yote yatafanyika kupitia TASAC," amesema Mhe. Kihenzile.

 

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika kuimarisha usalama wa usafiri majini ili kuongeza imani ya wawekezaji na kukuza uchumi wa buluu. Aidha, Naibu Waziri ameiagiza TASAC kuendelea kuwekeza katika rasilimali watu kwa kuongeza wataalamu wenye ujuzi na uzoefu ili kukidhi mahitaji ya sekta yanayotarajiwa kuongezeka kuelekea mwaka 2030.

 

Amesema ongezeko la shughuli za usafiri na biashara ya majini linahitaji wataalamu wa kutosha ili kuhakikisha huduma za ukaguzi, usimamizi na udhibiti wa usalama zinaendelea kutolewa kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.

 

Katika ziara hiyo, Mhe. Kihenzile pia ameipongeza TASAC kwa kuendelea kuimarisha utendaji wake, hatua iliyowezesha kuongeza gawio kwa Serikali kutoka Shilingi bilioni 16.37 hadi Shilingi bilioni 20.45, sawa na asilimia 15 ya mapato ghafi ya Shirika kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.

 

Amesema mafanikio hayo yanaakisi usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na mchango wa TASAC katika kuimarisha uchumi wa Taifa kupitia sekta ya usafiri wa majini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo